Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Polisi mjini Nakuru walitibua njama ya majangili waliokuwa wameteka nyara lori moja lililokuwa likisafirisha pembejeo kutoka Nairobi kuelekea Eldoret, katika kituo cha kibiashara cha Mbaruk viungani mwa mji huo.

Kulingana na naibu OCPD wa kituo cha polisi cha Central Janet Wasike, majangili hao watatu waliteka nyara dereva aliyekuwa akisafirisha pembejeo hiyo mwendo wa saa tano usiku wa Jumatatu.

Hata hivyo, polisi waliokuwa wakishika doria walishuku gari hilo ambalo tayari lilikuwa likitolewa pembejeo hiyo, na walipokaribia waporaji hao wakaanza kuwashambulia.

“Gari hilo lilikuwa limebeba magunia 240 ya pembejeo, kila gunia lilikuwa na kilo hamsini,” alisema Wasike.

Polisi walilazimika kujibu mashambulizi hayo, ambapo walikamata mmoja wa majambazi hao huku wawili wakitoweka.

Dereva wa gari husika hakujeruhiwa, huku polisi wakimzuilia jambazi huyo ili asaidie katika uchunguzi.

“Kama idara ya polisi, ni kazi yetu kuhakikisha uchunguzi unafanyika. Leo mshukiwa amefikishwa mahakamani, na tunatumai atasaidia kukamatwa kwa wenzake wawili,” alisema Wasike.

Gari husika sasa limo katika kituo cha polisi cha Mwariki.