Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mizozo kati ya wanyama na wakaazi wanaoishi karibu na mbuga za wanyama za Hellsgate na Longonot mjini Naivasha, imeendelea kuongeza huku shirika la KWS likilaumiwa kwa kutowajibika kupunguza visa hivyo.

Kulingana na wasemaji wa Jamii ya wamaasai, mizozo mingi inayotokea kati ya binadamu na wanyama pori, huhusisha wanyama wanaotoka kwenye mbuga ya kitaifa ya Hellsgate, ambapo wanaoathirika hutatizika kupata fidia kutoka kwa shirika la kulinda wanyama KWS.

Licha ya kushirikiana na usimamizi wa mbuga hilo katika uhifadhi wa mazingira, jamii hiyo inadai hakuna faida wanayopata kutoka kwa Hellsgate, huku wakitaka kuwekeana mkataba wa makubaliano ili kuhakikisha rasilimali hizo zinawafaidi wenyeji.

Mmoja wa viongozi wa jamii hiyo Jackson Ole Sencho, amesema wakati ambapo shirika hilo linafaa kuanza kutekeleza miradi ya kijamii umefika.

Akihutubia wanahabari mjini Naivasha Ijumaa, ole Sencho alisema: “Wanyama hao wamekuwa wakivamia wananchi na watoto wetu, na hasara tunayopata haifidiwi na KWS. Tunataka miradi ya kusaidia jamii kiuchumi, kwa sababu tunahusika na kulinda mazingira katika hifadhi ya hii.”