Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Jamii ya Maasai ambao wanajihusisha katika shughuli za biashara za kuuza bidhaa za rejareja katika jiji la Mombasa na vitongoji vyake, wametoa wito kwa serikali ya Kaunti ya Mombasa kuwatengenezea mahali na kujenga vibanda vya kufanyia biashara zao.

Vijana hao zaidi ya ishirini ambao walikutana katika eneo la umma la Mama Ngina Drive siku ya Jumamosi katika hafla ya kujadili mustakabali yao katika shughuli ya biashara walisema kuwa wamekuwa wakidhulumiwa na askari pamoja na maafisaa wa Kaunti.

Walisema maafisa hao hukusanya pesa za ushuru kwa kuwatia mbaroni na kuwazuilia na kuwapiga faini ya shilingi elfu kwa madai kuwa wanauza bidhaa bila kibali ilhali wanalipa kodi kwenye serikali hiyo.

Wakiongea na waandishi wa habari kwa uongozi wa John Ole Sepuk wafanyabiashara hao walisema kuwa unyanyasaji kutoka kwa maafisa wa Kaunti umesababisha hata baadhi yao kuaccha kazi hiyo ambayo wanasema ndio kitega uchumi chao.

Kundi hilo ambalo inajumuisha vijana ambao hujihusisha na kuuza bidhaa kama mishipi, bangili za kitamaduni za kuvaa mikononi pamoja na shanga na bidhaa nyingine, walisema serikali ya Kaunti ya Mombasa ikiongozwa na gavana Ali Joho sharti iwakumbuke kwa kuwajengea vibanda hivyo.

Walisema vibanda hivyo vitafanya rahisi kwao kutekeleza biashara zao na iwe mbinu moja nao wanachangia kulipia kaunti kodi.

“Sisi tunaomba serikali kutujengea vibanda angalau na sisi tuwe na mahali tumetulia tunapofanya biashara zetu ili tuchangie katika kukuza Kaunti yetu,” alisema kiongozi wao.