Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Jamii ya wapokomo imeelezea wasiwasi wao kuhusu jinsi zoezi la usajili wa wapiga kura katika Kaunti ya Tana River unavyoendeshwa.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa eneo la Galole Gassa, Bakari Kirigo, jamii hiyo ilidai kuwa kuna baadhi ya watu katika kaunti hiyo amabao wameanza kuwasafirisha wakaazi kutoka maeneo ya Kilifi, Malindi, Watamu na Lamu, na kuwaleta katika eneo hilo kusajiliwa kama wapiga kura ili kunyima jamii hiyo nafasi za uongozi.

Kwenye kikao na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatano, Kirigo alisema kuwa hali hiyo inafaa kusitishwa mara moj na Mshirikishi mkuu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC kanda ya Pwani Kazkazini Bi Amina Soud anafaa kuondolewa eneo hilo kwa madai ya kushindwa kuwajibikia majukumu yake.

Kirigo alisema kuwa iwapo swala hilo litakosa kuangaziwa, basi huenda likasababisha uhasama baina ya jamii hiyo na wale wanaosajiliwa katika kaunti hiyo, na kupendekeza kuwa hatua za dharura kuchukuliwa ili kuzuia mpango huo.

"Tunaitaka serikali kumuondoa huyo Kamishna kwa sababu ameshindwa kuwajibikia majukumu yake na kuruhusu wakaazi wa maeneo mengine kuja katika kaunti yetu na kujisajili kama wapiga kura. Swala hilo hatutalikubali kabisa na lazima hatua za dharura kuchukuliwa ili kusitisha mpango huo,” alieleza Kirigo.

Hatua hiyo inajiri huku zoezi la usajili wa wapiga kura kote nchini likiingia wiki yake ya tatu licha ya idadi ndogo ya wakazi wakijitokeza kisajiliwa.