Share news tips with us here at Hivisasa

Jamii ya Makonde walioingia eneo la Pwani mnamo mwaka wa 1936 kutoka Msumbiji sasa wameamua kujitengezea vitambulisho vyao baada ya shinikizo lao la kutaka kusajiliwa na serikali kuonekana kutofua dafu.

Jamii hiyo inayosema kuwa mababu zao walikuja maeneo ya Kwale na Mombasa baada ya kuahidiwa kazi katika mashamba ya makonge, lakini baada ya kandarasi hiyo kuisha, wakashindwa kurudi Msumbiji.

Akiongea na mwandishi wetu siku ya Jumanne mjini Mombasa, mwenyekiti wa muungano wa jamii hiyo Thomas Nguli alisema kuwa wamekuwa wakishinikiza serikali ya Kenya kuwasajili kama wakenya bila mafanikio, jambo lililowafanya kujitengezea vitambulisho vyao.

“Tumeongea na serikali pamoja na mashirika bado hatujapata haki, tumeamua kujitengezea vitambulisyo hivi vyetu kama jamii ya Makonde, na kama serikali inaona kuwa tunakosea basi watupe vitambulisho rasmi vya kitaifa,” alisema Nguli.

Aidha jamii hiyo inadai kuwa wamekuwa wakisumbuliwa na polisi kwa kukosa vitambulisho vya kitaifa kushindwa kuendelea na masomo kwa kukosa stakabadhi muhimu pamoja na kejeli kutoka kwa jamii zingine kwamba wao hawana nchi.