Naibu Kamishna wa kaunti ndogo ya Kisauni Julius Kavita ameeleza haja ya ushirikiano baina ya maafisa wa polisi, wazee wa nyumba kumi pamoja na wakazi wa eneo hilo kuimarisha usalama.
Akizungumza katika eneo la Kisauni mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Kavita alisema hatua hiyo huenda itasaidia kuondoa hofu kwa wenyeji, na hata pia wageni wanaopanga kuzuru eneo hilo msimu huu wa likizo kuendeleza utalii.
Kavita ameonya kuwachukulia hatua kali za kisheria watoto watakaopatikana wakiranda randa ovyo mitaani pamoja na wazazi watakaokosa kuwajibika, akisema asilimia kubwa ya wanafunzi wa eneo hilo hupachikwa mimba.
“Tunataka kuimarisha usalama kwa kushirikiana kama jamii na viongozi wetu ili kuona kwamba wageni wanaozuru eneo letu msimu huu wa sherehe za krismas na hasa mjini Mombasa wako salama,” alisema Kavita.
Afisa huyo tawala amepiga marufuku sherehe za 'disko' za usiku akisema kwamba kwa kiwango kikubwa zimezorotesha maendeleo ya eneo hilo.