Share news tips with us here at Hivisasa

Viongozi wa kidini, wazazi na jamii kwa jumla wamekosolewa kwa kutozungumzia wazi masuala ya ngono na athari zake, na kuchangia kukithiri kwa visa vya ubakaji katika eneo zima la Pwani.

Kulingana na Naibu Askofu wa Kanisa Katoliki jimbo kuu la Mombasa Padri Wilbard Lagho, visa vya ubakaji na dhulma za kijinsia katika eneo hilo vimekithiri mno kutokana na jamii kukosa ufahamu zaidi kuhusu athari za ubakaji na kutozungumzia msuala ya ngono.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Padri Lagho alisema kuwa ni wakati sasa kwa viongozi wa kidini, wazazi na jamii kwa jumla kujitokeza wazi wazi na kuhubiri mafunzo ya maadili mema ili kuwabadili vijana walio na fikra potovu ili kuwalinda watoto wa kike.

"Tunawashauri viongozi wa kidini, wazazi na jamii kwa jumla kuhakikisha kuwa wanazungumzia masuala ya ngono na kuwaelimisha vijana ili kuona kuwa visa vya ubakaji na ulawiti vinasitishwa kwa kiasi kikubwa,” alisema Lagho.

Kauli ya kiongozi huyo wa dini imejiri huku visa vya ubakaji na ulawiti katika jamii vionekana kukithiri mno katika kaunti ya Mombasa, Kwale, Kilifi na Taita Tavta.