Wanasema siasa ni mchezo mchafu, na hakuna uadui katika siasa. Hata hivyo miongoni mwa jamii za Kenya, tofauti za kisiasa kati ya viongozi wao wa ‘kikabila’ zimekuwa na adhari chungu nzima kwa maisha yao, ukabila ukikolea, ufisadi pamoja na chuki mitandaoni.
Ni hali iliyodhihirika wazi baada ya mwanasiasa, mwandishi wa vitabu na mbunge wa zamani wa Subukia Koigi wa Wamwere, kumkosoa kinara wa CORD katika mtandao wa kijamii wa Facebook, kwa kusema kwamba “Raila Odinga alifeli kwa kunyakua heshima ya mwanawe”.
Koigi anasema ilikuwa ‘aibu kubwa kwa Raila Odinga na gavana Joho wa Mombasa kuipa barabara hiyo jina la Fidel Odinga, kwa kuwa tu mwana wa Raila Odinga’ ambaye hakuna kubwa amefanyia Kenya.
Koigi, anasema kwenye maandishi hayo kwamba hata Fidel Castro wa Cuba ambapo jina la Fidel Odinga linatoka, hakuwahi ipa hata barabara moja jina lake, ambapo Koigi anahoji kama Odinga atakuwa na haki ya kumkosoa rais Uhuru Kenyatta, endapo ataamua kuupa uwanja mmoja wa ndege Kenya jina la mwanawe, au chuo vile vile.
Ni andiko hili ambalo kufikia Jumamosi saa sita, lilikuwa limefanya zaidi ya wakenya 400 kukwaruzana kwenye mtandao huo wa kijamii, likapata ‘Shares’ 390, na likes 100, wengine wakimkosoa kwa lugha kali, wengine wakimpa kongole, na wengine kumtania.
Monicah Kamau akasema: “Kongole bwana Koigi kwa mtazamo wako wa kizalendo”
Collins 'Gordy' Omondi naye akahoji: “Kwa hivyo sasa wangeiita barabara hiyo 'Koigi wa Wamwere’? Ni nini Lucy Kibaki na Mama Ngina walitufanyia ili taasisi na barabara zipewe majina yao? Ama ni sawa mradi tu hakuna ‘O’ kwenye majina yao? Huu ni ukabila.
Naye John Ndungu akasema: “Jambo ndogo tunalofaa kujadili kwa hekima, lakini wengine wetu wamelifanya swala la kikabila na kibinafsi”.
Hata hivyo Kifaru Mweusi alipasua mbarika kwa kuweka kwenye ukurasa huo cheti kinachosambazwa kwenye mitandao ya kijamii haswa Whatsapp, kudhihirisha jinsi serikali ya kaunti ya Mombasa ilivyotumia pesa za umma kufadhili shuguli nzima ya kubadilisha barabara hiyo jina.
“Kwa hivyo tupigane na ufisadi kwa kuwa wafisadi? Kweli nyani haoni lake. Mbona Pwani ilipie gharama yake (Odinga) ya ndege, hoteli na viburudisho?” Akahoji mkenya huyo.
Kufikia sasa gavana Joho amepuuzilia mbali madai ya cheti hicho, akisema Odinga aligharamia safari yake mwenyewe.