Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Chifu mmoja wa utawala kutoka Kaunti ya Nyamira amewaomba watu wanaoaminika kutokuwa wenyeji wa kijiji cha Riooga kujiwasilisha kwa hiari kwa maafisa wa polisi au wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Chifu huyo wa kata ndogo ya Riooga Peter Orina, aliyekuwa akizungumza siku ya Jumapili alipokuwa akiongoza hafla ya uandakishaji wa vitambulisho kwenye eneo hilo, alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kuthibiti visa vya ukosefu wa usalama kwenye soko la Mosobeti, huku akiongezea kuwa wananchi wengi walikuwa tayari wamewasilisha lalama zao kuhusiana na ukosefu wa usalama, hali ambayo imeilazimu serikali kuchukua hatua za dharura. 

"Ni kweli kuwa tunakumbana na visa vya ukosefu wa usalama, na mimi kama mwakilishi wa serikali nawasihi watu ambao sio wenyeji wa eneo hili kujiwasilisha kwa maafisa wa polisi kwa kuwa kupitia njia hiyo tutaweza kubaini ni akina nani wanaoishi hapa bila idhini," alisema Orina. 

Chifu huyo aliongeza kwa kuwasihi wakazi wageni lakini walio na vitambulisho kuwasilisha barua zao za kupewa idhini ya kuishi katika maeneo hayo ili waondolewe kwenye sajili ya watu wanaoishi katika eneo hilo bila kibali.

Aidha, alisisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kuthibiti tabia za watu wanaojihusisha na wizi, hali ambayo kufikia sasa imesababisha duka kumi kuvunjwa na bidhaa kuibwa kwenye soko la Mosobeti. 

"Natoa amri kwa wale watu walio na vitambulisho na wasio wenyeji wa eneo hili kuwasilisha stakabadhi rasmi zikaguliwe, na wakikosa kufanya hilo watachukuliwa hatua kali za kisheria kwa kuwa hali hii itatusaidia kuthibiti watu wenye tabia za wizi wa mara kwa mara kwenye soko la Mosobeti," alisisitiza Orina.