Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho ameikosoa serikali kufuatia jinsi maafisa wa Tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC walivyovamia afisi ya Kinara wa mrengo wa Cord Raila Odinga.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Joho alisema kwamba anastaajabishwa na jinsi serikali inatekeleza majukumu yake.

Alidai kuwa serikali imedhihirisha wazi kuwa imeshindwa kukabiliana na kashfa za ufisadi nchini.

Joho alisema kwamba serikali pamoja na Tume ya EACC zinafaa kuchunguza taarifa zinazotolewa na wananchi kuhusiana na kashfa za ufisadi badala ya kumshinikiza mwananchi kuchunguza taarifa hizo.

Aidha, Joho alisema kwamba EACC ni tume huru hivyo basi inafaa kuchukua jukumu lake kisheria.

Gavana huyo alisema kwamba kuwakandamiza Wakenya kwa kutoa habari muhumi kuhusu serikali ni kukiuka haki zao huku akiitaka tume ya EACC kufanya kazi yake kwa heshima.

"Tunaitaka serikali kukoma kumdhalilisha Raila Odinga kufuatia kashfa za Eurobond. Tume ya EACC lazima ichukue jukumu lake kikamilifu na kuchunguza jinsi pesa hizo zilivyotumiwa na kueleza wananchi,” alisema Joho.

Kauli ya Gavana huyo wa kaunti ya Mombasa imejiri baada a Kinara wa Mrengo wa Cord Raila Odinga kukosa kufika mbele ya Tume ya EACC kuandikisha taarifa kuhusu matamshi aliyotoa kuwa serikali imefuja shilingi bilioni 140 mkopo wa Eurobond.