Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho ameshikilia kuwa atapigania haki ya wakaazi wa shamba la Waitiki kuhusiana na suala la kulipa ada ya shilingi elfu 182 kwa shamba hilo kwa kila familia hadi serikali itakapoondoa mpango huo kwa wakaazi hao.

Akizungumza katika eneo la Kisauni mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Joho amesema kuwa ada hiyo iko juu zaidi na kulingana na hali ngumu ya maisha ya wakaazi wa eneo hilo kamwe hawafai kulipa ada hizo kwa ardhi zinazotolewa na serikali.

Joho amesema kuwa atahakikisha serikali imeliangazia vyema suala hilo ili kuona kwamba  masuala ya uskwota eneo la Pwani haya angaziwa kisiasa kwani hatua ya serikali kuitisha pesa kwa wananchi ili kulipa ada na kupewa hati miliki ni ukandamizaji na unyanyasaji wa haki za wananchi.

"Msimamo wangu ni ule ule kuwa wakaazi wa Shamba la Waitiki kuwa ayepewa ardhi na serikali hafai kulipa chochote, mwanzo pesa serikali inaitisha kwa wakaazi hao ni nyingi mno elfu 182 ikiwa mtu kupata elfu mbili ni ameangaika sana sasa hizo pesa zitatoka wapi na maisha yamekuwa magumu," alieleza Joho.

Kwa upande wake mwakilishi wa wanawake kaunti ya Mombasa Mishi Mboko amewakashifu viongozi wanaozidi kumkejeli Gavana Joho, akisema kuwa kamwe viongozi wa Mombasa hatasalia kimya wakiona gavana akirushiwa cheche za maneno hadhara huku akiwataka wakazi kutokubali kugawanywa kisiasa.

"Sisi kama viongozi wa Mombasa hatutakubali Gavana wetu kukejeliwa hadharani na wakaazi tafadhali msikubali kugawanywa kwa msingi ya kisiasa kuweni wanganwa ili tuweze kufanya maendeleo pamoja," alisema Mboko.