Wiki kadhaa baada ya hafla kubwa kuandaliwa wilayani Likoni kaunti ya Mombasa ambapo rais Uhuru Kenyatta alitoa hati miliki kwa maskwota wa shamba la Waitiki, Alhamisi ilikuwa siku ya kwanza gavana wa wa kaunti hiyo Hassan Joho kurudi tena eneo hilo baada ya ziara hiyo.
Licha ya kwamba alienda kwa minajili ya kuzindua miradi ya kimaendeleo, gavana Joho alichukua fursa hiyo kufungua wazi hisia zake kwa wakazi hao kuhusu shamba la Waitiki.
Joho aliwaambia maskwota hao kushikilia msimamo wao wa kususia kulipa ada iliyotolewa na serikali, ambapo hapo awali Rais Kenyatta alikuwa amewaambia kwamba ni lazma walipe.
Gavana huyo amewasisitizia maskwota hao kutolipa pesa hizo akisema kwamba ardhi hiyo ni ya Mombasa na wala hawafai kuangaishwa kwani hakuna mtu yeyote anayeimiliki.
“Shamba hili ni letu, hatutoki na tutaendelea kukaa hapa. Mimi nawaambia msilipe pesa hizo na tena nasisitiza msilipe,” alisema Joho.
Ameongeza kuwa serikali inafaa kuwapa wananchi wa Likoni uhuru wa kutekeleza maendelo katika eneo hilo, huku akiongeza kuwa agizo hilo la kulipa ada litalemaza shughuli zao za kiuchumi.
“Sisi tunataka kujenga hospitali hapa, kurekebisha barabara pamoja na miradi mingine kwa sababu tuna haki katika ardhi hii na ikiwa tutaanza tena mambo ya kulipa maendeleo yatarudi nyuma,” aliongeza.
Licha ya kwamba matamshi yake yalipokewa kwa shangwe, swali linalosalia ni iwapo maskwota hao watafuata agizo la rais au kile gavana walichoambiwa na gavana.