Gavana wa Kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho ametoa imani kwa wafuasi wa chama cha Cord kuwa kitashinda kiti cha ubunge cha Malindi na kusisitiza kuwa watafuata sheria kupata kiti hicho.
Gavana huyo amewasuta wale ambao wana imani potovu kuwa chama hicho kitatumia njia za mkato kupata kiti hicho cha ubunge na kuweka wazi kuwa siasa za eneo la Pwani ni za chama hicho cha upinzani na chama cha Jubilee hakina nafasi yoyote ya kunyakua nafasi hiyo.
Akiongea katika eneo la Malindi wakati wa kumtangaza rasmi mgombea teule ambaye atapeperusha bendera ya chama cha Cord, na kutangaza rasmi kwa wafuasi na wapiga kura wa eneo bunge hilo, Joho alisema kuwa chama cha Jubilee kijiweke tayari kwenye makabiliano ya siasa na kuongeza kuwa wana imani kuwa wapiga kura wa eneo hilo watampigia kura mgombea huyo mteule.
Chama hicho cha Cord kilimtangaza muwaniaji wao Willy Baraka Mtengo siku ya Jumanne.
Wakiongea na mwandishi huyu, baadhi ya wapiga kura pamoja na wakazi wa Kaunti ya Mombasa walitoa maoni yao wakisema kuwa chama cha ODM kitashinda kiti hicho cha ubunge hata ingawa Rais aliwapa zawadi kwa kumteua Dan Kazungu kuwa waziri kwenye serikali ya Jubilee mwezi jana baada ya kufanya mabadiliko kwenye baraza lake la mawaziri.