Ununuzi wa feri mbili mpya kutumika katika kivuko cha feri cha Likoni kamwe sio suluhu la kusitisha matatizo katika kivuko hicho kila uchao.
Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Ali Joho alisema hayo wakati wa sherehe za Jamhuri katika uwanja wa Tononoka mjini Mombasa siku ya Jumamosi, huku akisema kwamba lazima mbinu mbadala kuidhinishwa ikiwemo ujenzi wa daraja.
Kulingana na Joho, matukio ya hivi punde katika kivuko hicho yanaashiria wazi kuwa ununuzi wa feri mpya kamwe hautatua changamoto hizo, na akasisitiza kujengwa kwa daraja.
“Ununuzi wa feri mpya sioni kama itakuwa suluhisho la kusitisha misongamano na changamoto za kila uchao katika kivuto cha feri cha Likoni, lakini ujenzi wa daraja itakuwa suluhisho mwafaka kwa wakazi wanaotumia kivuko hicho,” alisema Joho.
Naye Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa amesema kwamba wasimamizi wa shirika la huduma za feri wamezembea na kuchangia kuathirika kwa sekta ya utalii na uchukuzi kati ya Mombasa na Pwani Kusini.
“Wasimamizi wa shirika la huduma za feri nchini ndio wamezembea kutekeleza majuku yao na kuchangia kuathirika kwa sekta ya utalii na iwapo hawabadili basi tutawashinikiza kujihuzulu,” alisema Marwa.