Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mbunge wa Ruaraka Tom Kajwang amemtaka rais Uhuru Kenyatta kukoma 'kutumia mamlaka yake vibaya' kwa kuchukua jukumu la kuandika sheria kinyume na katiba ya nchi.

Kulingana na Kajwang’, jukumu la kutunga za nchi limetengewa wabunge kwa mujibu wa katiba ya nchi ili kuona kwamba taifa hili linazingatia demokrasia na haki za kibinadamu.

Aliongezea kuwa iwapo atazidi kuandika sheria na kuwashinikiza wabunge kuzipitisha basi wakenya watazidi kukandamizwa.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamis katika kongamano la Muungano wa Jumuiya ya mawakili wanaohudumu katika mabunge ya Afrika, Kajwang’ alisema kwamba hali hiyo imechangiwa na washauri wakuu wa rais kwa kumuelekeza vibaya ili kuwafaidi baadhi ya watu flani.

Aidha, aliwataka mawakili wanaoshauri bunge la kitaifa pamoja na kamati ya kumshauri rais kutumia jukumu lao vyema kabla ya sheria hizo kuletwa bungeni kujadiliwa ili kuzuia taifa hili kutoangamia kiuchumi

“Wabunge wanalalamika kwamba rais anatumia mamlaka yake vibaya kutunga na kuandika sheria, hiyo ni kinyume na katiba ya nchi. Tunamtaka akome mara moja ili wakenya wafaidi na raslimali za nchi, na haya yote yanatokana na mawakili wanaomshauri pamoja na kamati yake ya kumshauri,” alisema Kajwang’.

Kongamano hilo la siku mbili linatarajiwa kukamilika hii leo, Ijumaa, baada ya muungano huo wa jumuiya ya mawakili wanaohudumu katika mabunge ya Afrika kukamilika na uchunguzi wa viongozi wapya.