Kiongozi wa muungano wa Cord Kalonzo Musyoka amesisitiza kuwa muungano huo haupo tayari kuvunja vyama vyake tanzu.
Akizungumza siku ya Jumapili katika uga wa umma wa Caltex katika eneo la Likoni, Kaunti ya Mombasa, Kalonzo alisema kuwa vyama vinavyounda muungano wa chama cha upinzani vitabaki vile vilivyo hadi uchaguzi mkuu ujao.
Kiongozi huyo alisema kuwa wale wanaofikiria kuwa muungano huo utavunjika watangoja mno, na kuwataka wafuasi wa upinzani kuendelea kuwaunga mkono.
Makamu wa rais huyo wa zamani ambaye aliandamana na seneta wa Kaunti ya Mombasa kwenye harakati za kuwarai wenyeji kujiandikisha kama wapiga kura aliwaonya wenyeji kuwa iwapo hawatajitokeza kujisajili kupiga kura, itakuwa vigumu kufanikisha maazimio yao ya kuiondoa serikali ya Jubilee kutoka mamlakani.
“Nawaomba wote mlio hapa mjitokeze kujiandikisha kupata kadi za kupiga kura, ili ikifika mwaka wa uchaguzi mkuu ujao, tuwaondoe Jubilee kutoka uongozini. Kura yenu ndio itatuwezesha kufanikisha hayo,” alisema Kalonzo.
Matamshi ya Kalonzo yaliungwa mkono na viongozi wengine wa muungano huo wa upinzani kutoka eneo la Pwani, wakiongozwa na Seneta wa Kaunti ya Mombasa Hassan Omar, ambaye aliwasisitizia wakazi umuhimu wa kujiandikisha kupiga kura ili kujiweka tayari kwenye uchaguzi wa 2017.