Share news tips with us here at Hivisasa

Kiongozi mwenza wa muungano wa upinzani wa Cord Kalonzo Musyoka amesisitiza kuwa muungano huo haupo tayari kuvunja vyama tanzu kama walivyofanya wapinzani wao kutoka sehemu ya serikali.

Akizungumza siku ya Jumapili katika uga wa umma wa Caltex, eneo la Likoni katika kaunti ya Mombasa, Kalonzo alisema kuwa vyama vinavyounda muungano wa chama cha upinzani vitabaki vile vilivyo hadi uchaguzi mkuu ujao.

Kiongozi huyo amewataka wale wanafikiria kuwa muungano huo utavunjika watangoja mno, na kuwataka wafuasi wa upinzani kuendelea kuwaunga mkono.

Makamu wa rais huyo wa zamani ambaye aliandamana na seneta wa kaunti ya Mombasa kwenye harakati za kuwarai wenyeji kujiandikisha kupiga kura aliwaonya wenyeji kuwa iwapo hawatajitokeza kujisajili kupiga kura, itakuwa vigumu kufanikisha maazimio yao ya kuiondoa serikali ya Jubilee kutoka mamlakani.

“Nawaomba wote mlio hapa mjitokeze kujiandikisha kwenye kupata kadi za kupiga kura, ili ikifika mwaka wa uchaguzi mkuu ujao tuwaondoa Jubilee kutoka uongozini, kura yenu ndio itatuwezesha kufanikisha hayo,” aliwarai kiongozi huyo wa upinzani.

Matamshi ya Kalonzo yaliungwa mkono na viongozi wengine wa muungano huo wa upinzani kutoka eneo la Pwani wakiongozwa na seneta wa kaunti ya Mombasa Hassan Omar, ambaye aliwasisitizia wakazi umuhimu wa kujiandikisha kupiga kura ili kujiweka tayari kwenye kivumbi cha mwaka wa uchaguzi 2017.