Kamati ya bajeti katika bunge la kaunti ya Nyamira na wananchi wa matabaka mbalimbali walijumuika kwenye mkahawa mmoja mjini nyamira kujadiliana kuhusu maandalizi mapya ya kiwango cha ushuru watakachokuwa wakilipa kwenye mwaka wa bajeti wa 2015-2016.
Akihutubu kwenye hafla hiyo, mwenyekiti wa kamati ya bajeti kwenye bunge la kaunti ya Nyamira James Sabwengi alisema kuwa mkutano huo ni wa muhimu mkubwa kwa kuwa makadirio ya bajeti hayawezi kupitishwa kwenye bunge la kaunti hiyo bila ya wadau kuhusishwa kwenye majadiliano.
"Mkutano huu ni wa maana kwa kuwa bila kuwahizisha wananchi kwa mujibu wa katiba, makadirio ya bajeti hayawezi kupitishwa kwenye bunge la kaunti, na kwa sababu hiyo, ningependa kuwahimiza wananchi waendelee kujitokeza kwa wingi kwa mikutano ijayo," alisema Sabwengi.
Sabwengi aliongeza kwa kusema ulipaji ushuru unafaa kuainishwa kwa usawa ili usije ukawaumiza wananchi wa kawaida au kusababisha serikali kutopokea ushuru wa kutosha, huku akiwahimiza wakazi kulipa ushuru kwa kuwa kwa muda sasa wananchi wa Nyamira wamekuwa wakilipa ushuru wa asilimia 2.5, hali inayoilazimu serikali ya kitaifa kufadhili miradi ya maendeleo kwenye kaunti hiyo.
"Ni jambo zuri kuainisha ulipaji ushuru ili kwamba tusije waumiza wananchi wa kawaida au kusababisha serikali kutopata ushuru wa kutosha kuendeleza miradi mbalimbali, na ningependa kuwahimiza wananchi kuendelea kulipa ushuru kwa kuwa asilimia 2.5 ya ushuru tunaolipa hautoshi kufadhili miradi, hali inayoilazimu serikali ya kitaifa kuingilia kati nakufadhili miradi huku," alisema Sabwengi.
Kwa upande wao, wananchi waliohudhuria mkutano huo walisema kuwa wako tayari kushirikiana na serikali ya kaunti hiyo ili kuhakikisha ushuru wakutosha unakusanywa.