Kamati ya Shule ya msingi ya Majaoni iliyoko Kisauni, Mombasa, imemtaka Waziri wa Elimu Dkt Fred Matiang'i, kumrejesha mwalimu mkuu wa shule hiyo aliyehamishwa kwa madai ya ufujaji wa pesa.
Kamati hiyo ya watu 11 lipiga kambi katika afisi za tume ya kuwaajiri walimu nchini (TSC) mjini Mombasa siku ya Jumatatu na kuapa kuwashawishi wazazi na wanafunzi kuandamana iwapo mwalimu huyo hatarejeshwa shuleni humo.
Welington Mwatsama ambaye alikuwa mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Majaoni, alihamishwa kwa shule jirana kama mwalimu wa kawaida siku chache tu baada ya Waziri wa Elimu Fred Matiang'i kufanya ziara ya ghafla katika shule hiyo mapema mwezi huu.
Kwa mjibu wa mkurugenzi wa TSC tawi la Mombasa, Ibrahim Rugut, Mwatsama, alishindwa kumuelezea waziri namna shilingi 240,000 zilivyotumika, jambo ambalo linaaminika kuwa chanzo cha uhamisho wake.
Hata hivyo, mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo Stephen Karanja, aliyakana madai hayo na kusema kuwa pesa hizo hazikuwa zimetumwa shuleni humo.
“Shule haikupokea pesa hizo waziri alizozitaja,” alisema Karanja.
Karanja aidha alisema wanakamati wako tayari kushirikiana na wazazi na wanafunzi ili kuishurutisha TSC kumrejesha mwalimu huyo.