Kamishna wa Kaunti ya Nyamira Josphine Onunga amewataka machifu na manaibu wao kutambua maeneo hatari, ili kudhibiti visa vya uhalifu katika kaunti hiyo.
Akihutubia wanahabari siku ya Alhamisi, Onunga alisema kuwa hali ya kutambua maeneo yanayokumbwa na visa vingi vya uhalifu itasaidia vyombo vya usalama katika kaunti hiyo kubaini maeneo yaliyo na mahitaji ya maafisa wengi wa usalama, na hata pia magari ya oparesheni.
"Tumekuwa tukipokea lalama kutoka kwa wakazi wa kaunti hii kuhusiana na visa vya ukosefu wa usalama, na ningependa kuwahakikishia wananchi kuwa maafisa wetu wa utawala hasa machifu na manaibu wao wanafahamu vyema maeneo yanayokumbwa na ukosefu wa usalama, na sharti wahakikishe visa hivyo vinakabiliwa," alisema Onunga.
Onunga aidha alishukuru umma kwa kushirikiana na vyombo vya usalama ili kudhibiti visa vya ukosefu wa usalama, huku akishtumu wahudumu wa bodaboda kwa mazoea ya kuchukua hatua mikononi mwao kwa kuwateketeza washukuwa wa uhalifu pindi wananchi wanapowakabili washukiwa hao.
"Ningependa kushukuru wananchi kwa kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutupa ripoti kuhusiana na uhalifu. Tutahakikisha kuwa ripoti yeyote tunayopewa tunaiweka siri. Ningependa pia kuwaonya wahudumu wa bodaboda walio na mazoea yakuteketeza washukiwa wa uhalifu," aliongezea Onunga.