Serikali ya Kaunti ya Mombasa itafanya uzinduzi rasmi wa kampeni ya usafi kwenye shule zote za umma katika eneo hilo siku ya Jumamosi.
Kampeni hiyo iliyopewa jina 'Mambo Safi' italenga kuwapa wanafunzi wa shule za msingi katika kaunti hiyo, mafunzo kuhusu jinsi ya kutunza mazingira ya shule zao pamoja na eneo zima la Mombasa.
Akiongea katika redio moja siku ya Alhamisi, mkuu wa idara ya mazingira katika kaunti hiyo Tendai Lewa alisema mpango huo ni moja katika ya agenda ambazo gavana wa kaunti hiyo alitoa wakati wa kampeni zake kwa wananchi.
“Tumegundua suluhu ya kutatua tatizo la uchafu wa mazingira ni kuanza kutoa mafunzo kwa wanafunzi wetu shuleni. Tutahakikisha mpango huu umefaulu,” alisema Lewa.
Mkuu huyo wa idara alisema kuwa watakuwa na zoezi la kufanya usafi katika shule zote za kaunti hiyo kila Jumamosi ya tatu ya kila mwezi, ambapo wanafunzi katika shule husika watajumuika kuzoa takataka.
Alisema kuwa pia wanafunzi hao watapewa mafunzo maalum kuhusu jinsi ya kugeuza takataka hizo hadi kutengeza vifaa ambavyo vitaweza kutumika.
Mbali na kuzoa takataka, Lewa alisemakuwa serikali ya kaunti itatoa miche kwa shule zote ili wanafunzi wapande miti kama njia mioja ya kuboresha mazingira.
“Gavana Hassan Joho wakati wa kampeni alisema kwamba atahakikisha takriban miti milioni moja imepandwa katika shule zote. Sasa tutauanzisha mpango huo ili kutimiza ahadi,” aliongeza Lewa.
Mpango wa 'Mambo Safi' unatarajiwa kuleta mabadiliko katika mazingira ya shule pamoja na eneo zima la Mombasa.
Lewa alisema kwamba watatumia shule zote za msingi za kaunti hiyo, ambazo zinakadiriwa kuwa zaidi ya 150.