Zaidi ya wafanyikazi 500 huenda wakapoteza ajira baada ya mabohari mawili ya kampuni ya Auto Port mjini Mombasa kufungwa katika hali ya kutatanisha.
Hatua hiyo imetokana na Maafisa wa Halmashauri ya Bandari ya Mombasa pamoja wale wa Halmashauri ya utozaji ushuru nchini kutoa agizo la kusitisha shughuli za ukaguzi na upakuaji wa mizigo katika mabohari hayo.
Akiongea na wanahabari nje ya afisi ya kampuni hiyo siku ya Alhamis, Afisa msimamizi wa oparesheni katika kampuni hiyo Hussein Ayub alikosoa hatua hiyo akisema kuwa maafisa hao hawajatoa ilani yoyote kabla ya kufunga shughuli za kampuni hiyo, huku akiitaka serikali kuu kuingilia katika ili kusitisha hatua hiyo kwani wakazi wengi huenda wakakosa ajira.
"Tumestajabishwa na hatua ya KPA na KRA jinsi maafisa wao walivyovamia kampuni yetu na kufunga shughuli zetu bandarini bila ya kutupatia ilani yoyote, hii ni hujuma na tutaelekea mahakamani kupinga hatua hiyo," alisema Ayub.
Kampuni hiyo inayodaiwa kumilikiwa na familia ya Gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho imedai kuelekea mahakamani kusitisha hatua hiyo wakidai kuwa maafisa hao walifaa kuwaeleza sababu muhimu za kufunga kampuni hiyo kabla ya kuchukua uamuzi huo.