Kampuni ya kutengeneza nguo ya EPZ inaendelea kushtumiwa kutokana na madai kwamba imekuwa na mazoea ya kuwanyanyasa wafanyikazi wake kila mara.
Haya yanajiri huku zaidi ya wafanyikazi elfu mbili wakiachishwa kazi katika kampuni hiyo iliyoko Mombasa.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Jimmy Odara mwakilishi wa wadi ya Changamwe, alisema kuwa sio mara ya kwanza kwa mgogoro wa aina hiyo kushuhudiwa katika kiwanda hicho.
“Kampuni ya EPZ imekuwa ikiwanyanyasa wafanyikazi wao kutoka zamani na imekuwa sasa kama mazowea. Huwezi kuwapiga watu kalamu kufuata utaratibu wa kisheria unaohitajika,” alisema Odara.
Wakati huo huo, mwakilishi wadi huyo alidai kuwa kampuni hiyo haifuati sheria za leba nchini jambo linalosababisha masaibu ya kila mara yanayoshuhudiwa.
Aidha, Odara aliyeandamana na wafanyikazi hao katika maandamano ya amani alishinikiza serikali kuu kudhibiti kampuni kama hizo ambazo zinawanyanyasa wananchi.
“Kampuni yoyote ikiwa inafanya biashara katika nchi yoyote lazima ifuate sheria za leba. EPZ imekuwa ikipuuza hilo na tunafahamu kwamba ni jukumu la serikali kufuatilia mambo haya,” alisema Odara.
Hata hivyo, wakili wa wafanyikazi hao Yusuf Mahamud Abubakar alisema kuwa kampuni hiyo ilifanya makosa kuwaachisha kazi bila notisi na kwamba wamewasilisha kesi kortini kupinga hatua hiyo.
Wakili huyo aliongeza kuwa wamewasilisha kesi katika mahakama ya viwanda Mombasa na watashinikiza warejeshwe kazini la sivyo wapewe fidia ili wajipange kuanzisha biashara zingine kujikimu kimaisha.
Kesi iliyowasilishwa imeahirishwa na itasikizwa tarehe Februari 26, 2016.