Share news tips with us here at Hivisasa

Zaidi ya wanachama 158 wa kampuni ya kununua ardhi ya Natoli(Natoli Land Buying Company) katika eneo la Ndabibi, Naivasha wameitaka serikali kuingilia kati na kutoa suluhu katika mzozo wa shamba lenye ukubwa wa ekari 16,400 wanaodai linapelekea madhara kila kuchao.

“Ningependa serikali itupe ulinzi katika shamba hilo ili kuzuia maafa zaidi kwa sababu maafa ambayo yanashuhudiwa pale huenda yakaongezeka,” Alisema mkurugenzi wa kampuni hiyo Jackson Ole Kateng’i.

Wanachama hao kutoka jamii ya wamaasai aidha wameshtumu madalali kuwa chanzo cha mzozo huo wakidai umepelekea maafa ya watu zaidi ya sita katika siku za maajuzi.

Wakiongea mjini Nakuru Jumatano walisema mmoja wa walioaga dunia angali hajazikwa kufuatia vuta nivute iliyoshudiwa wikendi kuhusu shamba hilo walilonuia kumzika mwendazake.

Wamewataja baadhi ya walaghai wanaosema wanatumia ukora kuwalaghai shamba lao walilolinunua miaka minne iliyopita kuchunguzwa wakihoji iwapo hatua ya haraka haitachukuliwa huenda madhara zaidi yakashuhudiwa kutokana na shamba hilo.

Wamezitaka wizara husika kuingilia kati wakihoji tangia kuwepo kwa madalali hao ndipo mzozo huo ulizuka wakihoji kuwa mbeleni walipolinunua shamba lao miaka minne iliyopita kutoka kampuni ya adc hali ilikuwa shwari kwao.

Kwa sasa wamewataka wanaokaa katika shamba hilo kuondolewa kwanza hadi pale hatma ya mzozo huo itakapobainika.