Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Idara ya Maji, Misitu na Mali asili katika kaunti ya Kilifi inapania kuweka mabomba ya maji yapatao kilomita 1, 700 ili kukabiliana na uhaba wa maji unaowahangaisha wakaazi wa kaunti hiyo, licha ya kaunti hiyo na zile za Mombsa na Kwale kukatiwa huduma za maji na bodi ya usambazaji maji Pwani.

Katibu katika idara hiyo, Andrew Makoti amesema kuwa mabomba hayo yatasambaza maji katika maeneo ambayo yalikuwa hayana maji, huku akiahidi kuihimiza bodi ya usambazaji maji Pwani kuunga mkono mradi huo na kusitisha tatizo la uhaba wa maji Kilifi.

Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatatu baada ya mkutano wa washikadau katika sekta ya maji Pwani, kwa ushirikiano na bodi ya usambazaji maji Pwani, Makoti alisema kuwa mradi huo ulioanzishwa miaka mitatu iliyopita unakadiriwa kukamilika ifikapo mwisho wa mwaka huu wa kifedha.

Alisema kuwa tayari fedha za kukamilisha mradi huo zimetengwa na shughuli hiyo inatayarajiwa kuanza rasmi mwezi Machi ili kuhakikisha kuwa uhaba wa maji Kilifi unasitishwa na kusaidia wakaazi wa kaunti hiyo kupata maji safi bila kulazimika kutembea mwendo mrefu.

“Tunatarajia kuanza mradi huu wa kuweka mabomba ya maji ya zaidi ya kilomita 1,700 ili kukabiliana na uhaba wa maji kwani maji ni muhimu kwa jamii. Tutaihusisha bodi kuu ya usambazaji maji Pwani ili shughuli hii isikumbwe na changamoto kutokana na kuwa mradi huu ni muhimu kwa jamii,” alisema Makoti.

Aidha, alisema kuwa kukosekana kwa sheria mwafaka ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira kumepelekea kucheleweshwa kuchukuliwa hatua kwa baadhi ya kampuni zinazochafua mazingira katika kaunti ya Kilifi.

“Tumepanga mikakati ya kukabiliana na baadhi ya makampuni yanayoharibu mazingira kwa sababu hatua hiyo ndio inacheleweshe mipango ya kukabiliana na uhaba wa maji. Tuko tayari kuhakikisha kuwa tunaekeza katika masuala ya mazingira na maji safi.