Share news tips with us here at Hivisasa

Kaunti ya Mombasa ni mojawapo ya kaunti tisa nchini ambazo zimeweza kufikisha na kupitisha kiwango cha ukusanyaji wa kodi kilichowekwa na serikali cha shilingi milioni mia saba na kumi na nane.

Takwimu za taasisi ya maswala ya uchumi (IEA) zinaonyesha kuwa katika mwaka uliotamatika wa 2015, Kaunti ya Nairobi imeongoza kwa ukusanyaji wa kodi kwa shilingi bilioni 11.6, ikifuatwa na Mombasa shilingi bilioni 2.5 na Nakuru shilingi bilioni 2.2

Kaunti hizi tatu zinaripotiwa kukusanya kiwango cha juu zaidi cha kodi kutokana na kuwepo kwa viwanda na sekta mbali mbali za utoaji huduma.

Sehemu kame na zilizo na jamii za wafugaji zimekuwa na kiwango cha chini zaidi ikiwa ni kaunti ya Marsabit, Mandera na Tana River.

Kaunti ndogo zaidi ambayo ni Lamu imekusanya shilingi million 62, na Tana River shilingi milioni 33.

Taasisi hiyo imesema kutokana na kaunti nyengine nchini kushindwa kufikisha kiwango hicho, sasa ni mzigo kwa serikali kuongeza fedha kwa ajili ya ugavi kwa serikali za kaunti.