Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Gavana wa Kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua ameelezea kuwa serikali ya kaunti yake itatumia milioni 55 ili kufadhili miradi mbalimbali ambayo inaanzaishwa na watu walemavu kutoka kila wadi ya kaunti hiyo.

Kulingana na gavana huyo, kila wadi itakabidhiwa takriban milioni moja kupitia hazina ya watu walemavu ili kufadhili vijana 1,000 wanaoishi na ulemavu.

"Lengo letu ni kuhakikisha kuwa vijana walemavu hawatengwi katika eneo hili. Kuanzia mwezi ujao, pesa hizi zitagawiwa wadi 55 kutoka kaunti hii ili vijana hawa wapate kujikimu maishani na kusahau shida zote walizopitia," Mbugua alielezea.

Gavana huyo alikuwa akizungumza siku ya Jumamosi katika ukimbi wa Menengai, ambapo pia alipokea vifaa 500 vya walemavu kutoka kwa shirika la Crunch for Africa Foundation yenye makao yake nchini Marekani.

Mbugua pia ameomba mashirika yenye uwezo kujitokeza kushirikiana nao katika kukuza vijana wasiojiweza na kuwasaidia kutimiza ndoto zao.

"Kama serikali tuko tayari kuungana na mashirika mengine ili kusaidia vijana hawa na wapate nafasi ya kuchangia katika ujenzi wa taifa," aliongeza Mbugua.

Mkurugenzi wa shirika hilo la Crunch for Africa Foundation David Hughes pia alihakikisha kuwa wataendelea kusaidia vijana walemavu ili kuwapa nafasi ya kujitegemea.

"Tuko na zaidi ya walemavu milioni 20 Barani Afrika na tutazidi kusaidia watu hawa ili wapate kuimarisha maisha yao pamoja na hali yao ya uchumi. Ombi letu ni kuwe na uongozi mwema ambayo itasaidia katika kuboresha maisha ya vijana hawa," Hughes alielezea.