Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya Kaunti ya Nyamira imelaumiwa kwa kusimamisha shughuli ya kupima ugonjwa wa saratani katika kaunti hiyo.

Hii ni baada ya idadi kubwa ya wakazi kujitokeza kupimwa ugonjwa wa saratani katika Hospitali ya Nyamira level five siku ya Alhamisi, na kupata shughuli hiyo imesimamishwa kwa sababu sisizojulikana.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika hospitali hiyo ya Nyamira, wakazi hao wakiongozwa na Joshua Nyakoe na Bethuel Osankia walilaumu serikali ya kaunti kwa kutoweka mikakati kabambe ya kuhakikisha kile walichokipanga awali kimefanywa kikamilifu.

Aidha, walisema wengi wao walitumia nauli kutoka makwao wakiwa na nia ya kupimwa ugonjwa wa saratani, huku nia yao ikigonga mwamba.

“Serikali ya kaunti imetukosea sana maana ilitangaza kuwa shughuli ya kupima ugonjwa wa saratani ingefanyika hapa Nyamira siku ya Alhamisi.Tumefika tukapata hakuna chochote kinaendelea,” alisema Joshua Nyakoe, mkazi.

Shughuli hiyo ya kupima ugonjwa wa saratani ilikuwa imefadhiliwa na serikali ya kaunti hiyo kwa ushirikiano na shirika la Health Care Rescue Centre.

“Uchunguzi wetu ambao tumefanya tangu tufike hapa umebaini kuwa serikali ya kaunti haikuwa na pesa za kulipia madaktari ambao walipaswa kutoa huduma hizo hoteli. Tunaomba serikali hii iwe inajipanga kikamilifu,” alisema Bethuel Osankia, mkazi.