Muungano wa wahudumu wa Tuktuk mjini Mombasa umeilaumu wizara ya uchukuzi na muundo msingi katika kaunti hiyo kufuatia sheria walizowekewa za uchukuzi bila ya kuwaarifu.
Akiongea na wanahabari huyo mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Mwenyekiti wa muungano huo Obedi Muruli alisema kuwa askari wa kaunti hiyo wamekuwa na desturi ya kushika madereva wa tuktuk kwa kutumia barabara ya Digo katikati mwa mji wa Mombasa kinyume na wanayofahamu wahudumu hao.
Obedi aliongeza kuwa askari hao wamekuwa wakiwapiga madereva hao wa Tuk tuk bila sababu zozote za kimsingi kinyume kabisa na sheria za nchi, huku akisema kuwa sheria inaeleza wazi mtu akipatikana na makosa anastahili kufikishwa mahakamani badala ya wao kudhalilisha.
Aidha, amesema kuwa hatua hiyo imewatia hofu wahudumu hao wanapoingia barabarani huku akiwalaumu askari hao wa kaunti pamoja na wale wa vifaa vya kuvuta magari yanapoharibika barabarani kwa kutoza faini ya juu zaidi ya shilingi elfu tano.
"Tunasikitishwa kuona askari wa kaunti wakipiga vijana wetu bila makosa kutokana na wao kuandamana wakilalamikia huduma duni na kubuniwa kwa sheria bila ya sisi kufahamishwa kama muungano," alisema Obedi.
Mwenyekiti huyo ameiomba serikali ya kaunti kuingilia kati swala hilo ili suluhu la kudumu kupatikana na madereva na kusitisha mgogoro huo wa mara kwa mara na kuishinikiza wizara hiyo kuwaarifu mapema sheria mpya za trafiki zilizoidhinishwa.
Wahudumu wa tuktuk mjini Mombasa wakiandamana kulalamikia unyanyasaji unaotekelezwa na maaskari wa kaunti pamoja na kubuniwa kwa sheria mpya za trafiki bila kufahamishwa.