Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya Kaunti ya Kisii imeombwa kuwaondoa watoto wanao randaranda mitaani mjini Kisii, kama njia moja ya kuondoa picha mbaya ya mjini huo.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne mjini Kisii, mwenyekiti wa wahudumu wa matatu mjini Kisii Samson Mose, alisema watoto hao huonyesha picha mbaya mjini humo.

Mose aliomba serikali ya kaunti kuwatafutia watoto hao makaazi pamoja na kuhakikisha kuwa wanapata elimu.

Aidha, mwenyekiti huyo alisema baadhi ya watoto hao huwa na tabia mbaya ya kuomba watu pesa kila wakati wanapopita, ama wanapokua wanatoka katika maduka ya jumla mjini humo.

“Tunaomba serikali ya Kaunti ya Kisii kujaribu kila iwezalo kuhakikisha kuwa watoto wote wanao randaranda mjini Kisii wanaondolewa na kupelekwa shuleni na kutafutiwa mahala pa kukaa,” alisema Mose.

Wakati huo huo, Mose aliomba serikali ya kitaifa na ile ya kaunti kushirikiana pamoja kuhakikisha usalama umeimarishwa mjini Kisii.

“Mji wa Kisii ni mji wa biashara kwa masaa 24 na kuna haja ya usalama kuimarishwa kila wakati,” alisema Mose.

Mose aidha aliomba madereva wa magari kuendelea kuzingatia sheria za barabarani wanapowasafirisha abiria, ili kupunguza visa vya ajali haswa msimu huu wa sherehe za krismasi na mwaka mpya.