Serikali ya Kaunti ya Mombasa imeshinikizwa kuibuka na mbinu mwafaka zaidi za kuyasafisha maji ya Bahari Hindi ili yatumiwe na wakaazi kwa kunywa majumbani mwao.
Kulingana na Msimamizi wa kundi la haki la maji lililo chini ya Halmashauri ya raslimali za maji nchini WARMA la ‘Mombasa water action group’ Grace Oloo, Kaunti ya Mombasa haina chemchemi ya maji na inategemea maji kutoka kaunti za Taita taveta, Kwale na ile ya Kilifi.
Oloo alisema kwamba ni lazima kwa serikali ya kaunti ya Mombasa kuibuka na mbinu ya kupata maji yake kwani swala hilo tayari Gavana wa kaunti Hassan Joho aliwahi lizungumzia katika manifesto yake kabla ya kuchaguliwa na wananchi kuwa gavana.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano katika afisi za kundi hilo, Oloo alisema kwamba sio tu kaunti ya Mombasa bali kaunti zote za Pwani zinapakana na Bahari hindi zinafaa kuifikiria kwa undani mbinu hiyo ili kulikabili tatizo sugu la maji.
"Tunawataka viongozi wa kaunti ya Mombasa kuharakisha mpango wa kusafisha maji ya bahari hindi kwani ni kati ya manifesto alizoahidi gavana Joho wakati wa kampeni ya uchaguzi uliyopita ili watu wa Mombasa tuwe na maji yetu na kuepukana na kukithiri kwa uhaba wa maji Mombasa,” alisema Oloo.
Aidha, aliitaka bodi kuu ya kusambaza maji eneo la Pwani kuwaeleza wakazi wa Ukanda huu kiini cha uhaba wa maji kuzikumba kaunti za Pwani, hususan Kaunti za Kwale Kilifi na Mombasa mara kwa mara.