Kenya itapata fursa ya kujiuza kitalii iwapo itafanikiwa kuandaa ziara ya wanadada kutoka Uingereza wanaocheza mchezo wa gofu ‘The ladies European tournament’ mwezi Novemba mwaka huu.
Katika mkutano wa maandalizi uliofanyika katika eneo la Vipingo ridge huko Kilifi siku ya Jumamosi, Waziri wa Utalii Najib Balala alisema kuwa Kenya itashirikiana na mataifa mengine ili kuona kwamba ziara hiyo inafanikiwa pakubwa kwa lengo la kuliuza taifa hili kitalii.
“Tunaimani kuwa shughuli hii iwapo itafanikiwa basi sekta ya utalii itaimarika kwa kiwango kikubwa. Tunatumai kupata soko kutoka nchi za magharibi,” alisema Balala.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa ziara hiyo ya ‘The ladies European tour’ Ivan Khodakash, alisema kwamba mchezo huo utaandaliwa katika mataifa 43 duniani na utawahusisha wanadada 312 na watazamaji takriban nusu bilioni kutoka nchi 85.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu wa Bodi ya utalii nchini Muriithi Ndegwa alisema kuwa iwapo ziara hiyo itafaulu, basi Kenya itakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kujiuza kitalii katika mataifa ya nje.
“Tunahitaji fedha hizo ili kuandaa mchezo huu kwani utatusaidia kwa kiwango kikubwa kuwavutia wageni na watalii kuzuru eneo letu. Hatua hiyo itaimarisha sekta yetu ya utalii sambamba na kuimarisha uchumi wa nchini,” alisema Ndegwa.
Kenya itahitaji kima cha shilingi milioni 124.8 katika maandalizi ya mchezo huo unaotarajiwa kufanyika kati ya tarehe 11 hadi 20 mwezi Novemba mwaka huu.