Vijana wa ukanda wa Pwani wamehimizwa kujitahadhari na wanasiasa wenye nia ya kuwatumia na kuwachochea kuvuruga amani hususan wakati huu ambapo joto la kisiasa linazidi kupanda Mkoani humo.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, katibu mtendaji wa baraza la maimam na wahubiri nchini, Sheikh Mohammed Khalifa, amewataka vijana kujiepusha na wanasiasa kama hao, na badala yake kujihusisha na masuala ya maendeleo yatakayowasaidia kupata riziki ya kila siku ili waweze kujikimu kimaisha.
Aidha, amewataka wanasiasa wa eneo la Pwani kuweka kando tofauti zao, kusitisha siasa za mapema na kujadaliana na serikali kuhusu namna ya kutatua shida zinazowakabili wakazi.
“Huu si wakati wa kupiga siasa, jambo la muhimu kwa sasa ni kuketi chini kama viongozi na kutafuta suluhu kwa shida zinazotukumba kama taifa,’’ alisema Khalifa.
Kauli ya Khalifa inajiri baada ya kuzuka tetesi kua kundi lililopigwa marufuku la MRC linapanga kuzua vurugu Mkoani Pwani baada ya baadhi ya wanachama wake kutiwa nguvuni.
Mapema mwezi huu, vijana mjini Mombasa walihusika katika rapsha na kusababisha wengine kujeruhiwa baada ya wafuasi wa seneta wa kaunti ya Nairobi Mike Sonko na wale wa Gavana Hassan Joho kukorofishana.