Balozi wa Amani humu nchini Grace Kibuku ametoa wito kwa wanasiasa kuhubiri amani hata wakati huu wa kampeni na usajili wa wapiga kura ili kuepuka vurugu miongoni mwa wananchi.
Kibuku anasema kuwa wakati huu wa usajili wa wapiga kura ni muhimu na wanasiasa wana wajibu wa kuhakikisha kwamba wakenya wanajisajili kwa wingi kama wapiga kura na kwamba wanadumisha amani wakati wowote.
"Ningependa kuwarai wanasiasa humu nchini wadumishe amani wakati huu wa shughuli ya kuwasajili wapiga kura ili kuepuka swala la migogoro," akasema Kibuku wakati wa mahojiano Jumanne mjini Nakuru.
Matamshi yake yanajiri siku moja tu baada ya baadhi ya ya wakaazi jijini Nairobi kujeruhiwa katika vurumai ya kusafirisha wapiga kura kutoka sehemu moja hadi nyingine.
Wakati huo huo, Kibuku, ambaye amaetangaza nia ya kuwania kiti cha mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Nakuru ametoa wito kwa wakazi wa kaunti ya Nakuru kuhakikisha kwamba wanadumisha amani wakati huu wa kupiga kura na hata katika kampeni zijazo.
Matamshi ya Kibuku yanajiri siku moja tu baada ya Kamishna wa kaunti ya Nakuru Joshua Nkanatha kutoa wito kwa wakazi kudumisha amani na kuhakikisha wanajisajili kwa wingi kama wapiga kura.