Mbunge wa Naivasha John Kihagi amempongeza waziri wa usalama wa ndani Joseph Nkaissery kwa kuingilia kati mzozo wa ardhi Naivasha.
Akizungumza Jumatano huko Naivasha, mbunge huyo alisema kuwa ni jambo la busara alilofanya Nkaissery.
"Ningependa kupongeza sana serikali kupitia wizara ya usalama wa ndani kwa kuingilia tatizo hili la ardhi ya Ng'ati na sasa haki imeanza kupatikana," alisema Kihagi aliyeandamana na waziri Nkaissery.
Itakumbukwa kuwa mzozo huo unatokana na hatua ya wakurugenzi wa shamba hilo kujaribu kuuza ekari elfu tatu ya shamba hilo bila kuwahusisha wanachama wote.
Hatua hiyo ilipelekea maandamano huku watu kadhaa wakitiwa mbaroni akiwemo mwakilishi wa eneo hilo Kariuki Mujini.
Hata hivyo, katika ziara yake eneo hilo, Waziri Nkaissery ameamuru wote waliotiwa mbaroni kuachiliwa huru bila kutozwa faini yoyote na hatua kuchukuliwa dhidi ya wakurugenzi wa shamba hilo.