Spika wa kaunti ya Nakuru Susan Kihika ametoa wito kwa wakaazi kuwasaidia wanaoishi na changamoto za ulemavu ili waweze kusajiliwa kama wapiga kura.
Katika mahojiano Jumatatu kwa njia ya simu, Spika Kihika amesema kuwa ni jambo la busara kwa jamii kufanya hivyo hasa kwa walio na changamoto ya kuona.
Alisema kuwa walemavu pia wana haki ya kusajiliwa na kushiriki uchaguzi mkuu ujao.
"Tunajua saa hii kuna shughuli ya kuwasajili wapiga kura na langu ni kuomba tu jamii kuhakikisha wanakumbatia walemavu na kuwasaidia wajisajili kama wapiga kura," aliongeza kuwa shughuli ya kupiga kura ni haki ya kila mmoja katika jamii na huanza na usajili wa watu.
Wakati huo huo, Spika Kihika amewataka akina mama na vijana katika kaunti ya Nakuru na taifa kwa jumla kuhakikisha wanajiandikisha kama wapiga kura ili kushiriki zoezi la kupiga kura mwaka ujao.
Kihika ameonyesha nia ya kuwania kiti cha useneta Nakuru 2017.