Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Afisa wa afya katika kaunti ya Nakuru Samwel Kingori, ametoa makataa ya siku 14 kwa vituo vyote vya kuuza maji mjini humo.

Hii ni kuhakikisha kwamba bidhaa hiyo muhimu inapitia katika maabara ya serikali kufanyiwa uchunguzi wa usafi kabla ya kuuzia wateja wao, wengi ambao ni wenye hoteli na maeneo ya chakula mjini.

Kingori akiongea Jumatatu na wanahabari mjini Nakuru alionya kwamba yeyote atakayefeli kutekeleza matakwa ya sheria kuhusu chakula, dawa na kemikali katika biashara hiyo, anahatarisha kukamatwa na kushtakiwa.

Maafisa wa afya Nakuru wamekuwa wakilalamikia hali ya maji mengi kutokuwa safi kwenye kaunti hiyo, kutokana na viwango vya juu vya kemikali aina ya floraidi.

Alisema maji mengi ya visiwa vilivyochimbwa kwenye kaunti hiyo haswa mjini Naivasha si safi kwa umma, kutokana na kuwa karibu na vyoo.

“Wanaouzia umma maji, ni lazima wahakikishe kwamba wanazingatia usafi. Ni lazima walete cheti cha kudhibitisha kwamba maji yao yamefanyiwa uchunguzi na maabara ya serikali kabla wa kuuzia umma maji hayo,” alisema King’ori.

Kulingana na notisi iliyotolewa tarehe Januari 6, 2016, pia madereva na makondakta wa magari ya mashirika ya kibinafsi ya kuuza maji watahitajika cheti cha afya.

King’ori alisema kwamba gari moja la kuuza maji lilipatikana mwaka jana likimwaga uchafu wa siwa katika uwanja wa Gioto hivyo kuhatarisha maisha ya watu.