Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Gavana wa kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua amekemea viongozi ambao amesema wameanza kufanya kampeni za uchaguzi wa mwaka wa 2017.

Akiongea mjini Elburgon siku ya Jumatano, Mbugua alisema kuwa kuna wanasiasa ambao wameanza kuzunguka kwenye kaunti hiyo wakirai wananchi kuwapigia kura.

Gavana huyo alisema huu si wakati wa siasa kwani muda wa viongozi waliochaguliwa haujakamilika.

“Kuna watu ambao wanazunguka wakifanya siasa na huu si wakati wa siasa. Siasa zikifika sote tutaanza kuwaambia wananchi yale tunataka,” Kinuthia alisema.

“Mnafaa kukataa kujihusisha na viongozi kama hao kwani kile wanafanya ni kutatiza maendeleo,” aliongeza. 

Kinuthia alikuwa ameandamana na viongozi kadhaa wa serikali yake wakati wa ziara hiyo ambapo alitoa msaada wa sare za shule kwa wanafunzi kutoka familia maskini. 

Viongozi kadhaa akiwemo mwenyekiti wa NACADA John Mututho tayari wametangaza azma ya kuwania ugavana kaunti ya Nakuru.