Siku chache tu baada ya Papa Francis kuondoka nchini, taifa la Kenya limebarikiwa tena kutembelewa na kiongozi mwingine wa kidini, safari hii neema ikiangukia wakazi wa Mombasa.
Kiongozi wa dini la Kihindu anayetambulika kwa kimombo kama 'His Divine Holiness Acharya Maharaja' aliwasili katika uwanja wa ndege wa Mombasa Jumatano asubuhi, lengo likiwa kueneza injili, amani na utangamano baina ya jamii mbalimbali nchini.
Baada ya kukaribishwa na viongozi na waumini wa dini la Kihindu wanaoishi ukanda wa Pwani akiwemo Sanghani Kaburu, Maharaja alisema ameleta ujumbe wa uwiano na upendo kwa wakenya na viongozi kwa jumla.
Kiongozi huyo atakuwa nchini kwa takribani juma moja, ambapo ataandaa msururu wa maombi kwa siku tatu mjini Mombasa kabla kuhamisha kambi kuenda Nairobi kwa shughuli sawia na hiyo.
Msafara wa Maharaja wenye ujumbe wa watu 10 ulilakiwa katika uwanja wa ndege wa Mombasa na kupewa ulinzi mkali na maafisa wa polisi.