Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kulizuka pata shika baina ya watu wa kutumia kivuko cha feri na waweka usalama katika kivuko hicho hii leo Jumanne, baada ya vijana wa usalama kumshika mtu mmoja na kudai kuwa alikuwa amebeba vifaa vya kuhatarisha usalama wa watu.

Kulingana na Charles Mate, ambaye alishuhudia kisa hicho kilichukua muda wa dakika 30, zogo hilo lilianzia upande wa pili wa kisiwani pale ambapo jamaa mmoja mwenye asili ya kigunya aliingia kwenye banda ya kungojea feri bila kufanyiwa ukaguzi kwenye eneo lililotengwa shughuli hiyo na kuhiari kupuuza wito wa waweka usalama.

“Huyo mwanaume aliingia tu kwenye banda la kusubiria feri na hakukaguliwa, lakini hakuwa amebeba vitu ila karatasi ya mkono, na hawa masoja walianza kumfuata hadi kwenye feri ndani na kutaka kumtoa kwa lazima, na watu hawakufurahi hali hiyo ya kumbeba mwenzao bila utaratibu, tukaanza kuwapigia kelele kwa vile hawakuwa na thibitisho ya kuwa na silaha,” alisema Mate.

Mkaazi mwingine, Jilo Mwalombe, aliwashtumu askari hao na kusema hawana mbinu ya uhusiano mwema, na wanatumia fujo wanaposhughulikia masuala yanapozuka baina yao na watumizi wa feri.

“Hawa masoja hawajui kuzinguma na watu, hata kama kitu kina umuhimu kwetu kama usalama, wao huja kwa fujo na kushika watu na kuanza kuwapiga bila ata kuwaelezea tatizo liko wapi,” alilalama Mwalombe.

Hata hivyo, askari mmoja ambaye aliongea na mwanahabari huyu na hakutaka kutajwa kwa jina alisema kuwa mwanaume huyo alipuuza kuwaonyesha alichokuwa amebeba kwenye mfuko aliokuwa nao na kukimbilia banbani.

Baadaye maafisa wa usalama kutoka idara ya utawala na ile ya kawaida waliingilia katika upande wa pili wa kivuko na kutuliza hali ambapo walimzuilia mshukiwa na kungojea hatima yake.