Muungano wa walimu nchini KNUT tawi la Nakuru, limetaka maafisa wakuu wa Tume ya kuwaajiri walimu TSC kupigwa kalamu kwa kukiuka amri ya rais na ile ya mahakama.
Mwenyekiti wa KNUT tawi la Nakuru, Njau Kuria amesema kuwa maafisa wakuu wa TSC wakiwemo mwenyekiti Lydia Nzomo na afisa mkuu metendaji Nancy Macharia wameonyesha ukaidi kwa rais kwa kukataa kuwalipa walimu mshahara wa mwezi wa Septemba licha ya kuagizwa kufanya hivyo.
Akizungumza na wanahabari siku ya Jumanne afisini mwake, Kuria alisema kuwa mazungumzo kati ya vyama vya walimu na TSC yatafanikiwa tu iwapo maafisa hao wawili wataondolewa afisini.
“Kama Rais na mahakama ya rufaa wametoa agizo, ni kwa nini TSC inakaidi agizo hilo? Sisi kama walimu tunataka Bi Macharia na Bi Nzomo waondolewe afisini kwa kuwa wameonyesha ukaidi sio tu kwa mahakama bali kwa rais,” alisema Kuria.
“Iwapo wawili hao wataendelea kukaa afisini basi waalimu wa Kenya watakosa haki yao na mvurutano utaendelea hata zaidi,”
Kuria alilitaka bunge kuanzisha mchakato wa kuwaondoa wawili hao afisini ili kuleta mabadilko katika tume hiyo kwa manufaa ya walimu na wanafunzi wa Kenya.
“Kama tume ya TSC inakumbwa na shida, ni walimu wa Kenya na wanafunzi watakao teseka. Ni jukumu la bunge kusafisha tume hiyo kwa kuwaondoa watu fulani kwa manufaa ya walimu na wanafunzi wa Kenya,” alisema Kuria.