Halmashauri ya Bandari nchini KPA imesema kuwa itafanya kazi kwa karibu mno na Mamlaka ya ushuru nchini KRA katika shughuli ya ukaguzi wa makasha katika Bandari ya Mombasa ili kuhakikisha kuwa bidhaa zote zinaoingia na kutoka nchini ni halali.
Kaimu Mkurugezi wa halmashauri hiyo ya KPA Catherine Wairi alisema kuwa shughuli hiyo itatekelezwa vyema katika Bandari ya Mombasa kuhakikisha kuwa hakuna mwekezaji ananyanyaswa na mali inayoingia katika bandari hiyo imezingatia sheria na viegezo vya bandari.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne, Wairi alisema kuwa kuingia na kusafirishwa kwa bidhaa za magendo katika bandari hiyo kumechangia kutofikia malengo ya bandari hiyo ya kuorodhesha makasha zaidi ya milioni mbili lakini juhudi zaidi zitaekezwa.
"Kama wasimamizi wa Bandari ya Mombasa tumeafikiana kushirikiana na KRA katika kuhakikisha kuwa shughuli ya ukaguzi wa mizigo katika bandari hii inatekelezwa vyema ili kuzuia kuingia kwa bidhaa za magendo bandarini,” alisema Wairi.
Kaimu Mkurugenzi huyo wa KPA alisema kuwa Kenya kwa sasa haina mipango ya kununua meli yake binafsi bila inafanya juhudi za kushirikiana na wamiliki wa meli za mizigo ulimwenguni kuhakikisha kuwa shughuli za kibaishara zinatekelezwa vyema na kuinua uchumi wa nchi.