Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Halmashauri ya ukusanyaji ushuru nchini KRA ilinasa shehena 16 za sukari katika Bandari ya Kilindini, siku ya Alhamisi, zinazodaiwa kuingizwa nchini kwa njia ya magendo.

Kwa mjibu wa kamishna wa KRA, John Njiraini, sukari hiyo inayokisiwa kuwa ya thamani ya shilingi milioni 28 iliingizwa nchini kutoka kwa kampuni moja ya sukari ya Uganda, na tayari ilikuwa imepakiwa kwenye bagi zenye nembo ya kampuni moja ya humu nchini.

“Tunashuku sukari hii iliingizwa nchini kupitia boda ya Kenya na Uganda kwa sababu kwa sasa tumeimarisha usalama katika vyombo vya majini,” alisema Njiraini.

Njiraini aliwakashifu wanaoiendeleza biashara ya magendo katika Bandari ya Mombasa kwa kile alichokitaja kama kukwepa kulipa ushuru.

Alisema kuwa hatua hiyo inanyima taifa hili mapato ambayo yangetumiwa kuboresha huduma kwa wananchi.

Aidha, afisa huyo alisema kuwa tayari uchunguzi umeanzishwa kubaini waliohusika katika biashara hiyo, na aliyelengwa kuzipokea bidhaa hizo, huku akisisitiza kuwa usimamizi wa KRA utazidisha juhudi za kuwanasa wanaopania kukwepa kulipa ushuru katika Bandari hiyo ya Mombasa.

Mapema mwezi huu, mamlaka ya KRA iliharibu zaidi ya magunia 130 ya mchele, na sukari yaliyodaiwa kuingizwa nchini kwa njia ya magendo.