Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakulima wa majani chai katika wadi ya Rigoma, Kaunti ya Nyamira wameomba halmashauri ya KTDA kukarabati barabara inayoelekea kituo cha ununuzi majani chai cha Embaro ili kuwarahisishia kazi.

Wakiongea na mwandishi huyu leo, Ijumaa katika wadi hiyo ya Rigoma,  wakulima hao wakiongozwa na mwenyekiti wa kituo hicho cha Embaro Emmanuel Orina walidai barabara inayoelekea katika kituo hicho ni mbovu zaidi, na hupelekea gari ya kuchukua majani chai kutofika kwa kituo hicho na kuwalazimisha wakulima hao kutembea mbali hadi kituo kingine cha Mochenwa ili kupima uzani wa majani chai yao.

Orina aliomba usaidizi ili barabara hiyo kukarabatiwa ili kurahisisha usafirishaji, badala ya wakulima kutembea mbali ili kupima majani chai yao.

“Tunaomba halmashauri ya KTDA kutusaidia na kukarabati barabara inayoelekea katika kituo cha kupima majani chai cha Embaro maana gari ya kubeba majaini chai halijawahi ingia hadi kituo hicho kufuatia barabara mbaya,” alihoji Orina.

“Kila siku tunapochuna majani chai huwa tunapelekea hadi kituo cha Mochenwa na tunashindwa kwa nini kituo chetu kilifunguliwa na hakitumiki,” alisema Orina.

Pia Orina na wakulima wengine waliomba serikali ya Kaunti ya Nyamira kushirikina na halmashauri hiyo kukarabati barabara hiyo ili gari ya kubeba majani chai kuwa rahisi na kufika katika kituo cha Embaro.