Share news tips with us here at Hivisasa

Muungano wa walimu wa Kuppet, tawi la Nakuru, umeonya afisi yake ya kitaifa dhidi ya kuingia katika mkataba na Tume ya TSC ya kuwajumuisha walimu hao chini ya bima ya afya, kinyume na walivyotaka.

Viongozi wa muungano huo wa Kuppet tawi la Nakuru wakiongozwa na mwenyekiti wa tawi hilo Sammy Kambo, katibu mkuu wa tawi hilo Gakau Mbugua na mweka hazina Rukwaro Theuri, wamekashifu afisi ya kitaifa ya chama hicho kwa kutotilia maanani yaliyoafikiwa katika mkutano wa kila mwaka, wa wajumbe wa chama hicho uliofanyika Bungoma mwaka jana, ambao ulipinga pendekezo hilo.

Akiwahutubia wanahabari siku ya Jumatatu mjini Nakuru, Mbugua alisema kwamba bima hiyo ya afya inawagharimu walimu fedha nyingi na kutokana na hilo, wanataka kuwekwa chini ya bima ya kitaifa ya afya ya NHIF.

“Tawi la Nakuru lilipinga mkataba huo ulioafikiwa mnamo Desemba 15, 2015 kati ya tume ya kuwaajiri walimu nchini TSC na chama cha Kuppet na wakaonelea ni vyema kwa kesi hiyo kusikilizwa mahakamani,” alisema Mbugua.

Mbugua alisema wanataka kurejeshewa fedha zao ambazo walitozwa kugharamia matibabu chini ya bima hiyo mpya mnamo mwezi Desemba, huku wakitaka malipo hayo kusitishwa mara moja.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa tawi hilo alisema kwamba iwapo hawatarejeshewa fedha hizo, wataelekea mahakamani.

Kambo alisema kuwa tume ya kuwaajiri walimu nchini TSC inawalazimu kujiunga na bima hiyo mpya badala ya ile ya kitaifa ya NHIF.

Alisema kuwa TSC na afisi ya kitaifa ya Kuppet zinafaa kujibidiisha kuhakikisha kuwa walimu wanapata nyongeza ya mishahara ya kati ya asilimia 50 na 60 kwa kuwa wanateseka kutokana na fedha zao kukatwa mara kwa mara.