Muungano wa walimu wa shule za upili na vyuo vikuu nchini Kuppet sasa umeitaki tume ya kuratibu mshahara wa wafanyikazi wa umma nchini SRC, kusitisha shughuli ya kutathmini mshahara wa walimu unaotarajiwa kuanza siku ya Jumanne.
Kwenye kikao na waandishi wa habari siku ya Jumatatu, mwenyekiti wa Kuppet, Omboko Milemba, alisema kuwa muungano huo utawasilisha kesi mahakamani kupinga shughuli hiyo iwapo SRC haitaweka wazi vigezo itakavyotumia kubaini mshahara wanayofaa kupata walimu kila mwezi.
Milemba alimlaumi mwenyekiti wa SRC, Sarah Serem, kwa kile alichokitaja kama kudinda kuuhusisha Kuppet katika shughuli hiyo licha ya muungano huo kutaka kujua hadhari ambayo matokeo ya uratibaji wa mshahara huo utaleta kwa walimu.
“Tunahofia huenda shughuli hiyo ikawa kikwazo kwa nyongeza ya mshahara ambayo walimu wamepigania kwa miaka mingi bila mafanikio,” alisema Milemba.
Kwa upande wake, Tume hiyo ya kuratibu mshahara wa wafanyikazi wa umma nchini SRC, ilisema kuwa uratibaji wa mshahara unalenga kuainisha mshahara wa wafanyikazi nchini kulingana na kazi zao na masomo yao.