Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Ukosefu wa ushirikiano wa kutosha baina ya wakuu wa usalama kaunti ya Lamu umetajwa kuwa chanzo cha idara ya usalama kaunti hiyo kushindwa kukabili kundi la Al-shabab lililovamia eneo la Mpeketono mwaka jana.

Haya ni kulingana na aliyekuwa kamanda mkuu wa polisi kaunti ya Lamu, Leonard Omollo alipokuwa akitoa ushahidi wake siku ya Jumatano katika mahakama kuu ya Mombasa, kwenye kesi ya ugaidi inayowakabili Mahadi Salim na Diana Suleiman.

Omollo aliiambia mahaka kuwa baadhi ya makamanda wa vikosi vya usalama walidinda kushirikiana naye kwa wakati ufaao kulikabili kundi la Al-shabab, jambo alilolitaja kusababisha kutoa nafasi kwa magaidi hao kutekeleza mashambulizi zaidi na kutoroka.

Aidha, aliongeza kuwa baadhi ya makamanda walisema waliogopa kushambuliwa na magaidi hao na kutoa mfano wa uvamizi wa Baragoi ambako maafisa wengi waliuwawa.

Vilevile alisema kuwa ukosefu wa mitambo ya mawasiliano kwa idara ya usalama kaunti ya Lamu ndio chanzo cha ukosefu wa mawasiliano kati ya polisi eneo hilo, jambo alilolitaja kuwa changamoto kubwa ya kueneza ujumbe baina ya maafisa wa usalama.

Itakumbukwa kuwa Juni 15, 2014 kundi la Alshabab lilivamia eneo la Mpeketoni na kusababisha mauwaji ya watu zaidi ya 60.