Jamii ya Lions Club Nakuru imetoa mchango wa bidhaa za thamani ya shilingi 250 elfu kuwafaidi wakimbizi wa ndani kwa ndani katika eneo la subukia.
Akizungumza katika ukumbi wa shule ya Lions Nakuru wakati wa kukabidhi bidhaa hizo kwa serikali ya kaunti ya Nakuru,Rais wa Lions Club Nakuru Lion Parvi Shah amesema kuwa bidhaa hizo zimetolewa a wanachama wa jamii ya Nakuru Lions Club katika juhudi za kuwasaidia wasiyojiweza katika jamii.
''Ningependa kuwafahamisha kwamba bidhaa hizi zimetolewa na wanachama hawa wa Nakuru Lions Club kama njia mojawapo wa kudhihirisha upendo kwa wasiyojiweza katika jamii''akasema Purvi Shah.
Bidhaa hizo zinajumuisha vyakula na blanketi miongoni mwa vitu vingine ambavyo vitasafirishwa hadi kambi ya wakimbizi huko subukia.
Lion Purvi Shah ameongeza kuwa jamii ya Lions Club Nakuru imejitolea kuwasaidia wasiyojiweza katika jamii kaunti ya Nakuru.
Wakati huo huo ametoa wito kwa Gavana Kinuthia Mbugua kuhakikisha kwamba barabara inayoelekea katika shule za Lions inakarabatiwa kwani ina umuhimu mno katika jamii hiyo.
''Bwana Gavana ningependa kukuomba tafadhali utusaidie kukarabati barabara hii inayoelekea katika shule zetu tatu za Lions kwani ni ya umuhimu sana''akasema Purvi Shah.
Kwa upande wake Gavana Mbugua aliwashukuru jamii ya Lions Club Nakuru kwa mchango wao katika jamii huku akisema kuwa serikali ya kaunti ya Nakuru itazidi kushirikiana nao katika kuimarisha maisha ya wakaazi.