Maafisa wa usalama eneo la Pwani wamewatia nguvuni washukiwa wawili wa ugaidi Mohammed Abdulrahman Mohammed na Zakaria Mohammed Athman katika eneo la Kipini kaunti ya Lamu katika operesheni ya kusaka magaidi.
Kwenye kikao na wanahabari katika makao makuu ya idara ya usalama eneo la Pwani mjini Mombasa siku ya Jumatano, Mshirikishi Mkuu wa Serikali ya kitaifa ukanda wa Pwani Nelson Marwa amesema kuwa magaidi hao walikamatwa katika eneo la Kipini na kushurutishwa kufichua maficho ya magaidi hali iliyopelekea kuwepo na makabiliano makali.
Marwa amesema kuwa makabiliano hayo yalitokea katika eneo la Kwachocha mjini Malindi ngome kuu ya magaidi hao na kupelekea kuuwawa kwa magaidi wengine wanne ikiwemo Issah Jabir, Abdallah Salim Marumu aka Dagas, Suleiman Awadhi aka Naksh na Zakaria Mohammed Athman huku magaidi wengine wakifanikiwa kutoroka na majeruhi mabaya ikiwemo Mohammed Abdulrahman Mohammed.
"Maafisa wa usalama wamefanikiwa kuwaua magaidi wanne kwa kuwapiga risasi katika makabiliano makali eneo la Kwachocha na wengine wakafanikia kutoroka wakiwa na majeruhi mabaya, usalama lazima uimarishwe katika eneo la Pwani, hilo tunawahakikisha wananchi," alisema Marwa.
Afisa huyo Tawala ameeleza kuwa maafisa wa usalama walifanikiwa kupata ghurunedi 5, pistul moja, Kipatakilishi kimoja, Vitambulisho 10, Simu za rununu 10, nakala ya kuonyesha eneo la Ijara, pamoja na Kuran.
Makabiliano hayo yalitokea asubuhi ya Alhamisi katika eneo hilo la Kwachocha mjini Malindi huku wakazi wakitakiwa kutokwa na hofu ya kiusalama kwani usalama wa eneo la Pwani umeimarishwa kuhakiksiha kuwa wananchi wanaishi kwa amani.