Share news tips with us here at Hivisasa

Wafanyikazi wa serikali ambao wameanza kujiunga na masuala ya kisiasa kufuatia kukaribia kwa uchaguzi mkuu ujao, wameonywa dhidi ya kufanya siasa kinyume na maadili ya kisiasa.

Akihutubia wakazi kule Bogichora siku ya Jumanne Dkt Evans Nyatigo, alisema kuwa maafisa wa mashirika ya kiserikali ambao wameonyesha nia ya kuwania nyadhifa mbalimbali za kisiasa wanastahili kujiuzulu kabla ya kuwania nyadhifa hizo.

"Kuna maafisa wengi wa mashirika ya serikali wanaoendelea kufanya siasa kwa kujipigia upatu wa nyadhifa mbalimbali za kisiasa. Kwa kweli hilo halifai kwa kuwa ni kinyume cha katiba maana wanafaa kujiuzulu kabla ya kushiriki siasa," alisema Nyatigo.

Nyatigo ambaye ana nia ya kuwania Ugavana katika Kaunti ya Nyamira kwenye uchaguzi wa mwaka wa 2017 alisema kuwa kampeni za mapema za wanasiasa wanaowania nyadhifa mbalimbali huenda zikazua mkanganyiko wa kisiasa miongoni mwa wapiga kura.

Alisema kuwa huenda hali hiyo ikawafungia nje wawaniaji wengine.

"Kuna sheria zinazostahili kufuatwa kuhusiana na uchaguzi na hizi kampeni za mapema hueda zikawakanganya wapiga kura na huenda baadhi ya maafisa hawa wakafungiwa nje kutoka kwenye vinyanganyiro vya nyadhifa za kisiasa," alisema Nyatigo.